BUKOBA SPORTS

Wednesday, June 11, 2014

KLABU YA COASTAL UNION KUFANYA MKUTANO MKUU JUNI 22 MWAKA HUU.


KLABU ya Coastal Union inatarajiwa kufanya mkutano mkuu wa mwaka wa wanachama utakaofanyika kwenye ukumbi wa Hotel ya Mkonge mkoani Tanga Juni 22 mwaka huu ambao utakuwa na agenda kuu mbili muhimu zitakazo jadiliwa na mengineyo. Akizungumza jana,ofisa Habari wa timu ya Coastal Union,Oscar Assenga alisema kwenye mkutano huo utakuwa na agenda mbalimbali lakini ya kwanza itakuwa ni kupokea taarifa na kujadili taarifa za kazi kutoka kamati mbalimbali za utendaji ndani ya klabu hiyo kwa kipindi kilichopita. Assenga alisema pamoja na hayo lakini kutakuwa na kuthibitisha bajeti kwa mwaka wa fedha unaofuata baada ya mwaka uliopita kumalizika ambapo mkutano huo hautaruhusu wanachama wanaodaiwa madeni kuhudhuria.
Aidha alisema pia watafanya marekebisho ya katiba kwa kuongeza kifungu cha kamati ya maadili ambapo hilo likiwa ni agizo la shirikisho la soka hapa nchini kwa mujibu wa maelekezo kutoka shirikisho la soka nchini. “Pia tutafanya marekebisho ya katiba kwani tutaongeza kifungu cha kamati ya maadili ambacho ni muhimu ikiwa ni agizo la shirikisho la soka nchini (TFF) “Alisema Assenga. Hata hivyo aliwataka wanachama waliopo sehemu mbalimbali hapa nchini kuhakikisha wanatimiza haki yao ya msingi kwa kuhudhuria kwenye mkutano huo muhimu kwa ajili ya maendeleo ya timu hiyo kongwe hapa nchini.

No comments:

Post a Comment