BUKOBA SPORTS

Wednesday, June 11, 2014

WAZEE WAJA JUU, WAKEMEA WENZAO WANAOMPINGA MANJI - YANGA!

BARAZA LA WAZEE wa Klabu ya Yanga hii Leo limeongea na Wanahabari na kukemea Wanachama wanaosema kwamba watapeleka Barua TFF kuushitaki Uongozi kwa kudai wamevunja Katiba kwa kujiongezea Mwaka mmoja zaidi madarakani.
Katibu wa Baraza la Wazee, Ibrahim Akilimali, amesema kwa niaba ya Baraza la Wazee wanasema Wanachama wanaopinga maamuzi ya Mkutano Mkuu uliokuwa na Wanachama zaidi ya 1500 basi wafuate taratibu za kuwasilisha malalamiko yao na si kufanya vinginevyo.
Mzee Akilimali alieleza: “Mwenyekiti wetu Yusuf Manji alishasema tangu mapema ya kwamba yeye hatagombea tena na Siku ya Mkutano aliyasema hayo awali, lakini Mjumbe wa Baraza wa Wadhamini mzee Jabir Katundu aliwasilisha hoja ya kumuomba aendelee na uongozi, ndipo Wanachama walipopata nafasi ya kujadili chini ya Mama Karume na kwa pamoja kuafiki Mwenyekiti aendelee japo kwa miaka minane!"


Akilimali aliongeza na kusema kwamba Manji hakuafikiana na suala hilo na ndipo alipoomba japo aongezewe muda wa Mwaka mmoja kabla ya kuelekea kwenye mikikimikiki ya Uchaguzi ili aweze kukamilisha baadhi ya mambo kama ya usajili, ujio wa Kocha Mkuu mpya Marcio Maximo na Ujenzi wa Uwanja.
Naye Mwenyekiti wa Baraza la Vijana Bw Bakili Makele amesema: “Sisi kama Vijana pia tunashangazwa hao baadhi ya Wanachama ambao wanataka kuirudisha Yanga nyuma, mara hii wameshasahau shuruba tulizopitia mpaka kufikia muafaka, sisi kama vijana tunasema hatuamini kama hao wanaosema hawakubaliani na maamuizi ya mkutano ni watu wanaoitakia mema klabu yetu!”
Aliongeza: "Mwenyekiti Bw Yusuf Manji hajayapenda madaraka na wala haitaji kuendelea kuiongoza Yanga, bali kwa maombi yetu sisi Wanachama pamoja na Baraza la Wadhamini alikubali kuiongoza japo kwa Mwaka mmoja kabla ya kuelekea kwenye Mkutano Mkuu wa Uchaguzi ambapo atakayejiona ana uwezo wa kuongoza Yanga basi atapata fursa hiyo ya kujinadi na si kupiga kelele sasa hivi kweye vyombo vya habari!"

No comments:

Post a Comment