WAKATA miwa wa Kaitaba, Kagera Sugar FC wamesema sasa wameiva kuivaa Azam fc katika mchezo wa kiporo wa ligi kuu soka Tanzania bara utakaopigwa leo Katika Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.
Kocha msaidizi wa ‘Wanankurukumbi’ hao, Murage Kabange amesema baada ya kutandikwa bao 1-0 dhidi ya Mbeya City jumamosi iliyopita, hawatakubali kuacha pointi tatu kwa mara nyingine mbele ya mabingwa watetezi.
“Tumejipanga, tumezungumza na vijana, tumewajenga kiakili na muda wote asubuhi tumefanya mazoezi mepesi, tuna matumaini kwamba kesho tutfanya vizuri katika mchezo huo ambao utakuwa mgumu kwasababu wenzetu walikotoka wamepata matokeo, kwahiyo wamekuja na nguvu ya kupata pointi tatu ambazo ni muhimu kwao”.
Wakati huo huo Azam fc wamefanya mazoezi asubuhi uwanja wa CCM Kirumba kuweka miili sawa kabla ya mechi ya leo.
Meneja wa klabu hiyo, Jemedari Said Mzumari amesema wamekusudia kuchukua pointi sita kanda ya Ziwa na kumalizia za Simba Dar es salaam, kisha kwenda Lubumbashi, DR Congo tayari kwa maandalizi ya ligi ya mabingwa.
Azam waliibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya wenyeji Stand United katika mechi ya ligi kuu iliyopigwa jumamosi uwanja wa CCM Kambarage, Shinyanga.
Kagera Sugar wakifanya mazoezi kwenye Uwanja wa CCM Kirumba Mwanza
No comments:
Post a Comment