BUKOBA SPORTS

Saturday, April 11, 2015

MAMBO YAMEIVA: DIDIER KAVUMBAGU MALI YA YANGA

Straika wa Azam FC, Didier Kavumbagu.
Wilbert Molandi na Sweetbert Lukonge
MAMBO yameiva kwani hadi sasa Yanga ina asilimia 80 za kumsajili straika wa Azam FC, Didier Kavumbagu na kudhihirisha kwamba fedha wakati mwingine inaweza kuwa si lolote katika uamuzi.Kavumbagu amebakiza mwezi mmoja tu kumaliza mkataba wake na Azam aliyojiunga nayo mwaka jana akitokea Yanga, hivyo sasa anarejea nyumbani.

Mabosi wa Yanga wameshafanya mazungumzo na Kavumbagu ambaye ameonyesha nia kubwa ya kurudi Yanga ili kuendeleza makali yake.
Kwa mujibu wa chanzo cha habari kutoka ndani ya Yanga, kwa asilimia 80 wameshamalizana na straika huyo baada ya kufikia makubaliano mazuri ya kurejea Jangwani.

Chanzo hicho kilisema, mshambuliaji huyo mwenyewe ana mapenzi na nia kubwa ya kurejea Yanga msimu ujao huku ikielezwa kuwa, kocha wa timu hiyo, Mholanzi, Hans van Der Pluijm, ameuambia uongozi ufanye lolote linalowezekana kuhakikisha Kavumbagu anasajiliwa.

“Naomba nikuhakikishie tu, Kavumbagu ana asilimia 80 za kusaini mkataba wa kuichezea Yanga msimu ujao, sasa tulichobakiza ni kusaini tu na sisi kumpa haki yake aliyotaka, wala hakuna tatizo juu ya usajili wake na wala msisikilize maneno ya Azam.

“Azam wanadai wamempa mkataba lakini siyo kweli, kwani mchezaji mwenyewe ametuhakikishia hajapewa mkataba wowote na timu yake, hivyo tuna nafasi ya kumsajili,” alisema mmoja wa vigogo wa kamati ya usajili ya Yanga.
Mmoja wa marafiki wa Kavumbagu, aliliambia Championi Jumamosi kuwa, straika huyo ana uwezekano mkubwa wa kurejea Yanga kwani anaamini anakosa vitu vingi kutoka kwa mashabiki na wanachama wa timu hiyo.

Hata hivyo, alipotafutwa Kavumbagu anayeshika nafasi ya pili kwa ufungaji katika Ligi Kuu Bara akiwa na mabao kumi, alisema: “Nipo Morogoro na kesho (leo) tunacheza na Mtibwa, hayo mambo tuyaache kwanza kwani akili yangu nimeielekeza katika mechi hii, ila nakuhakikishia hakuna timu niliyosaini mkataba hadi sasa.”

Kwa upande wake, Kocha wa Azam, George Nsimbe ‘Best’ alisema: “Siwezi kukubali kumpoteza Kavumbagu kwani ni mchezaji muhimu kikosini, nitaueleza uongozi usikubali aondoke kirahisi.”
CHANZO: CHAMPIONI JUMAMOSI

No comments:

Post a Comment