MSANII wa Bongo Fleva, Khadija Shabani Taya au Keisha ameibuka mshindi kwenye kura za maoni za Ubunge wa Viti Maalum kundi la Walemavu mkoa wa Dodoma na kuwa mshindi wa kwanza.
Keisha amepata kura 340 huku Stella Fueda akimfuatia kwa kupata kura 112, Anna Fungo kura 100 na Graceana Kavishe kura 54.
Jumla ya kura 721 zilipigwa, ambapo kura 75 ziliharibika na kura za halali zilikuwa 646.
Msanii huyo aliwahi kuhojiwa na vyombo vya habari na kubainisha kuwa, japo ni mlemavu wa ngozi lakini anajikubali, anajipenda, kujiamini na amekuwa akipigania amani ambayo wanastahili kuipata kutoka nchini.
Alisema alipoanza kuweka picha zake za siasa kwenye mtandao kuna baadhi ya watu walimpongeza na wapo waliosema kuwa hana uchungu na wenzake kwani waliamini anaingia kwenye siasa kwa nia ya kujinufaisha.
“Wapo wanaohisi nimeingia huku kwa ajili ya kujinufaisha mwenyewe mimi ni mpiganaji na ndio maana siku zote nimekuwa nikiwaza kuhusu amani yetu,” alisema.
Alisema fimbo ya mbali haiui nyoka na kidole kimoja hakivunji chawa akimaanisha kuwa lazima kusimamia sheria ambazo zitatusaidia kuendeleza amani, hivyo basi lazima kuwe na wawakilishi wa kutosha ndani ya Bunge na sauti zisikike ili sheria kutungwa na kutekelezwa pia.
Hiyo ni hatua ya kwanza ya mchakato wa kusaka nafasi ya kuwakilisha walemavu, ambapo sasa ataenda katika inayofuata ambayo itahusishwa washindi kutoka maeneo mbalimbali ya nchi.
No comments:
Post a Comment