BUKOBA SPORTS

Saturday, June 4, 2016

AFCON 2017: TANZANIA YATUPWA NJE, MISRI HAOO WATINGA FAINALI!


TAIFA Stars imeaga rasmi katika mbio za kuwania kufuzu michuano ya Mataifa ya Afrika (Afcon), itakayofanyika mwakani nchini Gabon.
Safari ya Stars imehitimishwa leo, baada ya kufungwa mabao 2-0 na Misri kwenye mchezo uliopigwa Uwanja wa Taifa Dar es Salaam, ukiwa ni mchezo wa kundi G.
Matokeo hayo yanawafanya Misri wamalize mechi za Kundi G wakiwa na pointi 10 baada ya mechi nne, wakishinda tatu na kutoka sare moja, wakati Tanzania inabaki na pointi yake moja na inashika mkia nyuma ya Nigeria yenye pointi mbili.
Stars ilikuwa na kibarua kigumu, kwani ilikuwa inatakiwa kushinda mabao zaidi ya 3-0 dhidi ya Mafarao hao ili iweze kufuzu kwa michuano hiyo kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1980.
Katika mchezo wa kwanza dhidi ya Misri uliopigwa jijini Alexandria, Stars ilifungwa mabao 3-0 na baada ya kujitoa kwa Chad katika kundi hilo la G, Stars ilikuwa na karata moja ya kutakiwa kuifunga Misri ili iweze kufufua matumaini ya kufuzu kwa michuano hiyo.

Katika mchezo wa leo, Stars walianza kwa kasi wakitawala katika dakika 20 za mwanzo, lakini kutokana na umakini wao mdogo wakashindwa kupenya safu ya ulinzi ya Misri.

Misri walianza kuhesabu bao la kwanza katika dakika ya 43 lililofungwa na Mohamed Salah, baada ya kupiga mpira wa faulo iliyosababishwa na Haji Mwinyi na shuti lake lilikwenda moja kwa moja wavuni.
Kipindi cha pili kilianza kwa Misri kufanya mabadiliko kwa kumtoa Mohamed Ibrahim na kumuingiza Amr Mohsen.
Nahodha wa Stars, Mbwana Samatta anayecheza soka la kulipwa nchini Ubelgiji katika Klabu ya Genk, alikosa penalti katika dakika ya 53 baada ya Himid Mao kuchezewa rafu ndani ya eneo la hatari na Mohsen.
Misri ilipata bao lake la pili katika dakika ya 58, mfungaji akiwa ni yule yule, Salah ambaye anaichezea Klabu ya AS Roma ya Italia, baada ya kumzidi mbio beki Aggrey Moris.


Stars, licha ya kufanya mabadiliko katika dakika ya 61 kwa kumuingiza John Bocco ambaye alichukua nafasi ya Elias Maguli, lakini hadi kipenga cha mwisho kinalia hawakuweza kupenya ngome ya Misiri na matokeo kubakiwa kuwa 2-0.
Stars: Deo Munishi ‘Dida’, Juma Abdul, Mwinyi Mngwali/Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ dk68, Aggrey Morris, Erasto Nyoni, Himid Mao, Thomas Ulimwengu/Deus Kaseke dk73, Mwinyi Kazimoto, Elias Maguli/John Bocco dk62, Mbwana Samatta na Farid Mussa.
Misri: Essam Kamal Tawfik, Alg Gabr Mossad, Ramy Hisham Abdel, Mohamed Abdel Sayed, Abood Abdulrahamn Amed, Tarek Hamad Hamed, Mohamed Nasser Elsayed, Mohamem Ahmed Ibrahim, Abdallah Mahamoud Said na Nagram Mohsin Fahmy.

No comments:

Post a Comment