Wakati mwili wa Mwanahabari, Mpoki Bukuku ukiagwa leo jijini Dar es Salaam, Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi ametuma salamu za rambirambi kwa Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri (TEF), Theophil Makunga kutokana na kifo hicho.
Mpoki Bukuku alifariki dunia Ijumaa iliyopita, alipokuwa akipatiwa matibabu kwenye Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Dar es Salaam alikokuwa akipatiwa matibabu baada ya kujeruhiwa vibaya kwa kugongwa na gari eneo la ITV Barabara ya Bagamoyo jijini.
Hadi mauti yanamkuta akiwa na umri wa miaka 44, Mpoki alikuwa Mpigapicha wa magazeti ya The Guardian ambako kabla aliwahi kufanya kazi kwa mafanikio makubwa katika kampuni za Mwananchi Communications na Business Times – zote za Dar es Salaam.
Rais Malinzi alipokea taarifa za kifo cha mwanahabari huyo kwa masikitiko makubwa na katika salamu za rambirambi pia zimekwenda kwa familia ya marehemu Mpoki Bukuku, ndugu, jamaa na marafiki na kuwataka kuwa na moyo wa subira wakati huu mgumu wa msiba wa mpendwa wao.
Rais Malinzi alimwelezea Mpoki Bukuku, wakati wa uhai wake alikuwa na mchango mkubwa katika tasnia ya habari za michezo akitoa mawazo yake hivyo ameacha alama ya ucheshi, kujituma na uwajibikaji katika kufanikisha kazi zake katika vyombo vya habari alivyofanyia kazi.
Mwenyezi Mungu aipumzishe roho ya marehemu Mpiki Bukuku mahala pema peponi.
Bwana alitoa, Bwana ametwaa, jina la Bwana lihimidiwe.
IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)
No comments:
Post a Comment