SIMBA leo imeifunga Ruvu Shooting, bao 1-0 na kuongeza gapu la pointi nne dhidi ya Yanga kwenye mchezo uliochezwa Uwanja wa Uhuru Dar es Salaam.
Vinara hao hawatacheza mchezo mwingine wa ligi mpaka yatakapo malizika mashindano ya Mapinduzi yatakayoanza visiwani Zanzibar kesho hadi Januari 13 sambamba na timu za Yanga na Azam huku wakiwa na pointi 44.
Simba walimiliki sehemu kubwa ya mchezo huo katika kipindi cha kwanza na kufanya mashambulizi kadhaa langoni mwa Ruvu lakini safu ya ulinzi ya Maafande hao iliyokuwa chini ya nahodha Damas Makwaya na Renatus Msesa ilikuwa imara kudhibiti mikikimikiki ya Wekundu hao.
Mohammed Ibrahim aliifungia Simba bao pekee dakika za nyongeza za kipindi cha kwanza kwa shuti kali la mguu wa kushoto ndani ya 18 baada ya kupokea pasi ya Janvier Bokungu.
Mshambuliaji mpya wa Simba anayecheza kwa mkopo klabuni hapo akitokea Zesco ya Zambia, Juma Liuzio alionyesha kiwango kizuri na kuwafanya mabeki wa Ruvu kuwa nae macho sambamba na Pastory Athanas ambaye katika mechi mbili za ligi alizocheza ameonekana kuwa mchezaji muhimu.
Mwamuzi Alex Mahagi kutoka jijini Mwanza aliwaonya kwa kadi ya njano Jabir Aziz, Bidii Hussein wa Ruvu huku Bokungu akionyeshwa kwa upande wa Simba.
Kocha Malale Hamsini wa Ruvu aliwapumzisha Ismail Mohammed na Jabir na kuwaingiza Shaban Msala na Chande Mahoja aligeuka kuwa mwiba mkali kwa wekundu wa Msimbazi akionyesha uwezo mkubwa wa kupora mipira na kuanzisha mashambulizi.
Kwa upande wa Joseph Omog aliwaingiza Liuzio, Mwinyi Kazimoto na Saidi Ndemla kuchukua nafasi za Bokungu, Ibrahim pamoja Shiza Kichuya.
No comments:
Post a Comment