BUKOBA SPORTS

Saturday, January 14, 2017

BARCELONA YAMTIMUA AFISA WAO ALIEDAI LIONEL MESSI SI LOLOTE BILA INIESTA NA NEYMAR!

MABINGWA Watetezi wa La Liga huko Spain, FC Barcelona, Leo watatinga kwao Nou Camp kucheza na Las Palmas huku wakigubikwa na mzozo uliohitimishwa kwa kufukuzwa kazi Afisa wao mmoja aliedai Supastaa wao Lionel Messi si lolote bila kuwepo kwa Wachezaji wenake Iniesta na Neymar.
Barca, ambao sasa wana Pointi 35 kwenye La Liga, wanashikilia Nafasi ya 3 nyuma ya Sevilla wenye Pointi 36 na Vinara Real Madrid wana Pointi 40 wakiwa wamecheza Mechi 1 pungufu.
Mzozo huo wa kumkanya Messi unamhusisha Pere Gratacós, Mchezaji wa zamani wa Barcelona B ambae ni Afisa Uhusiano hapo Barca, ambae akiongea na Tovuti ya huko Spain, Sport, alisema: “Messi asingekuwa mzuri kama alivyo bila ya Iniesta, Neymar na wenzao. Ni kweli ni bora!”
Kauli hiyo pengine imekuja muda usio muafaka kwani hivi sasa Barca inahaha jinsi ya kumwongezea Messi Mkataba na Mshahara kitu ambacho ni kigumu kwao kwa vile wanabanwa na Kanuni za La Liga zinazotaka Bajeti ya Klabu isizidi Asuilimia yake 70 kwa kulipa Mishahara.
Kwa sasa, Mkataba wa Messi unaokwisha baada ya Miezi 18, unampa Mshahara wa Euro Milioni 22 kwa Mwaka baada kukatwa Kodi.
Lakini wenzake, Neymar na Luis Suarez, ambao hivi karibuni walisaini Dili Mpya zinazoisha 2021, wanazoa kitita cha Euro Milioni 25 kwa Mwaka baada ya Kodi.
Mkataba wa Messi unamalizika Tarehe 30 Juni 2018 na baada ya hapo yupo huru kuondoka bila Barca kulipwa hata Senti.
Taarifa ya FC Barcelona kuhusu mzozo wa Pere Gratacós ilitamka kuwa Afisa huyo amefukuzwa wadhifa wake kwa kutoa maoni ambayo yanapingana na msimamo wa Klabu.

No comments:

Post a Comment