BUKOBA SPORTS

Saturday, November 4, 2023

BONDIA YUSUF CHANGARAWE ATWAA MEDALI YA FEDHA


Changalawe na Rais wa TBF

Na Rahel Pallangyo
BONDIA wa Tanzania, Yusuf Changarawe amepata medali ya fedha baada ya kushindwa pambano lake la fainali la mashindano ya kusaka nafasi ya kushiriki Michezo ya Olimpiki itakayofanyika Paris, Ufaransa 2024.

Changarawe alipigwa na bondia kutoka Misri, Abdelrahman Abdelgawwad katika pambano la uzito wa kilo 80 na hivyo kukosa nafasi ya kuiwakilisha Afrika katika Michezo ya Olimpiki.

Bondia huyo na wengine wa Tanzania sasa watasubiri mashindano mengine mawili yatakayofanyika Italia na Thailand Februari na Aprili mwakani ili kusaka tena nafasi ya kwenda Paris katika Olimpiki.

Tanzania katika mashindano hayo ya kufuzu huko Dakar, Senegal ilipeleka mabondia sita, wanne wa kiume na wawili wa kike, ambao walikwenda kusaka nafasi ya kwenda Paris.

Mbali na Changarawe, mabondia wengine wa Tanzania ni Musa Malegesi (kilo 92), Mwalami Salum (kilo 57) na Abdallah Mohamed (kilo 51) wakati wanawake ni Zulfa Macho (kilo 50) na Grace Mwakamele (kilo 60).

Mkuu wa msafara wa timu hiyo alikuwa Rais wa Shirikisho la Ndondi Tanzania (BFT), Lukelo Wilillo. Viongozi wengine ni Mashaga (kocha msaidizi), Samuel Kapunga (Kocha Mkuu) na Aisha George (matroni).

No comments:

Post a Comment