BUKOBA SPORTS

Tuesday, November 13, 2012

JERAHA LA JOHN TERRY LAZUA SHAKA STAMFORD BRIDGE, WENDA AKARUDI RAUNDI YA PILI YA MSIMU 2012/2013

Nahodha wa Chelsea John Tery akiugulia maumivu baada ya kugongana na mshambuliaji wa Liverpool, Luis Suarez katika pambano la Ligi Kuu lililoisha kwa sare ya bao 1-1 kwenye Uwanja wa Stamford Bridge juzi.

Terry akikatiza uwanja kutoka nje akitembea kwa msaada wa magongo, kufuatia kuumia goti la mguu wa kulia kama linavyoonekana. Anatarajia kuwa nje ya uwanja kwa mwezi mmoja.
LONDON, England

"Tunalazimika kusubiri hadi afanyiwe uchunguzi kujua ukubwa
 kamili wa jeraha lake.
Kuna wasiwasi mkubwa miongoni mwetu. Tulifurahishwa na 
marejeo yake dimbani baada ya adhabu. Tuna matumaini kwamba hatokuwa na jeraha kubwa sana"

LICHA ya vipimo kuonesha kuwa hajapata majeraha makubwa 
- na hivyo kudaiwa kuwa anaweza kukaa nje ya dimba kwa 
takribani wiki tatu hadi nne, mabingwa wa soka barani Ulaya, 
Chelsea chini  ya
kocha wake Roberto Di Matteo, wameingiwa na wasiwasi mkubwa wakihofu huenda nahodha wake John Terry, akaigharimu timu yake 
kwa kukaa nje ya dimba muda mrefu.



Terry alifunga bao la ufunguzi wa pambano hilo kali la Ligi Kuu ya England kabla ya kutolewa akiwa kwenye machela – baada ya kugongana na mshambuliaji Luis Suarez, ambaye alifunga bao la kusawazisha la Wekundu wa Anfield katika kipindi cha pili katika pambano la Ligi kwenye Uwanja wa Stamford Bridge.
Beki huyo wa kati wa Chelsea, ambaye alikuwa akirejea kwa mara 
ya kwanza akitoka kumaliza adhabu ya kufungiwa kucheza mechi 
nne kwa tuhuma za kumbagua Anthon Ferdinand, jana Jumatatu 
alifanyiwa vipimo kujua ukubwa wa jeraha, ambapo imeelezwa atakosekana dimbani kwa muda mfupi, ingawa klabu imeingia
 mchecheto.

akizungumza juzi kabla ya vipimo vya jana, Di Matteo alisema: "Tunalazimika kusubiri hadi afanyiwe kipimo kujua ukubwa kamili
 wa jeraha lake," alisema kocha huyo aliyerithi mikoba ya Andre Villas-Boas klabuni hapo.

"Kuna wasiwasi mkubwa miongoni mwetu. Tulifurahishwa na 
marejeo yake dimbani baada ya adhabu.

"Tuna matumaini kwamba hatokuwa na jeraha kubwa sana, lakini
 tutaona itakavyokuwa. Wakati wachezaji wanapoathiriwa kwa 
kiwango hicho, inatia shaka miongoni mwetu. Yuko katika maumivu
 makali hivi sasa."

Terry aliifungia bao la uongozi The Blues kunako dakika ya 20 ya 
pambano hilo, wakati kichwa chake cha nguvu kilipotinga nyavuni
 moja kwa moja akiunganisha kona ya Juan Mata na kuweka rekodi 
ya kuifungia Chelsea bao la 50.

"Aliuanza vema mno mchezo, akaonesha ubora wake dimbani,
 uzoefu na ushawishi mkubwa," alisema Di Matteo akimuelezea
 Terry katika mechi hiyo na kuongeza: "Tuna tumani hatokuwa
 nje ya dimba muda mrefu."

No comments:

Post a Comment