Mabao kutoka kwa straika wa kimataifa wa Burundi, Didier Kavumbagu na straika wa Uganda, Hamis Kiiza yaliipandisha Yanga kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara baada ya kuibuka na ushindi 'mtamu' wa mabao 2-0 dhidi ya Azam kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam huku mahasimu wao wa jadi, Simba wakipata kipigo cha ugenini cha 2-0 kutoka kwa Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro leo.

Kama ilivyokuwa kwa Yanga, Mtibwa walifunga mabao yao pia katika kila kipindi kupitia kwa mastraika wao nyota, Said Mkopi na Hussein Javu ambaye aliwahi pia kuiliza Yanga kwa kupiga 'hat-trick' wakati 'Wanajangwani' walipolala3-0 katika mechi yao ya raundi za mwanzo wa msimu.

Katika mechi ya Taifa, Yanga walionyesha soka safi kuanzia mwanzo wa mechi hadi mwisho, wakigongeana pasi za kuvutia na kutawala mno katika eneo la katikati ya dimba lililokuwa chini ya himaya ya kiungo wao wa kimataifa kutoka Rwanda, Haruna Niyonzima 'Fabregas'.
Kavumbagu ambaye sasa anaongoza katika orodha ya wanaowania kiatu cha dhahabu baada ya kufikisha magoli saba, aliifungia Yanga bao la utangulizi katika dakika ya tisa, akimalizia gonga safi baina ya Niyonzima, Simon Msuva na Mbuyu Twite na Kiiza alifunga goli la pili ambacho Azam walipotea kabisa na kutumia muda mwingi 'kuusaka mpira kwa tochi' kutokana na 'gonga' za kusisimua zaidi za Yanga; zikiwamo zilizozaa bao la Kiiza ambalo pia lilitokana na "one-two' za Niyonzima, Kiiza mwenyewe na Chuji kabla mfungaji kukwamisha mpira wavuni.

Kipigo cha leo kwa Simba inayoonekana kama ilitangulia na "baiskeli ya barafu" ni muendelezo wa matokeo yasiyoridhisha kwa timu hiyo kila inapocheza ugenini kwani licha ya kuongoza kwa muda mrefu kutokana na ushindi mfululizo wa mechi zao nyingi za nyumbani; mabingwa hao watetezi walishashikiliwa kwa sare pia katika mechi dhidi ya Coastal Union na Mgambo JKT jijini Tanga, sare dhidi ya Kagera Sugar waliyocheza nayo kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam na pia wakasimamishwa ugenini kwa sare isiyotarajiwa kwenye Uwanja wa Jamhuri, Morogoro dhidi ya 'maafande' wa Polisi Moro ambao hadi sasa ndiyo wanaoburuta mkia kwenye msimamo wa ligi hiyo.
No comments:
Post a Comment