Release No. 115
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Julai 14, 2013
MECHI YA TAIFA STARS, UGANDA YAINGIZA MIL 113/-

Mechi ya kwanza mchujo ya kuwania tiketi
ya kucheza Fainali za Afrika kwa Wachezaji wa Ligi za Ndani (CHAN) kati
ya Tanzania (Taifa Stars) na Uganda (The Cranes) iliyochezwa jana
(Julai 13 mwaka huu) imeingiza sh. 113,268,000 kutokana na watazamaji
17,121.

Tiketi za kushuhudia mechi hiyo ziliuzwa kwa sh. 5,000, sh. 7,000, sh. 10,000, sh. 15,000, sh. 20,000 na sh. 30,000.
Mgawanyo wa mapato hayo ulikuwa kama
ifuatavyo; asilimia 18 ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ni sh.
17,278,169.49 wakati wa gharama za uchapaji tiketi ni sh. 7,809,104.
Asilimia 15 ya uwanja sh. 13,227,108.98,
asilimia 20 ya gharama za mechi sh. 17,636,145.30 na asilimia 5 ya
Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) sh. 4,409,036.33.
Asilimia 60 ya Shirikisho la Mpira wa
Miguu Tanzania (TFF) sh. 52,908,435.91 na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa
wa Dar es Salaam (DRFA) sh. 2,645,421.80 ambayo ni asilimia 5 kutoka
kwenye mgawo wa TFF.
TAIFA STARS KAMBINI TENA JULAI 4
Timu ya Taifa (Taifa Stars) imeondoka
leo asubuhi (Julai 14 mwaka huu) kwenda Mwanza ambapo itapiga kambi ya
siku kumi kujiandaa kwa mechi ya marudiano dhidi ya Uganda (The Cranes)
kutafuta tiketi ya kucheza Fainali za Afrika kwa Wachezaji wa Ndani
(CHAN) zitakazofanyika mwakani nchini Afrika Kusini.
Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro
Premium Lager imeondoka kwa ndege ya PrecisionAir na itafikia hoteli ya
La Kairo wakati mazoezi yatafanyika Uwanja wa CCM Kirumba kulingana na
programu ya Kocha Mkuu Kim Poulsen.
Wachezaji walioko katika kikosi hicho ni
Juma Kaseja, Aggrey Morris, Mwadini Ally, Ally Mustafa, Shomari
Kapombe, Kevin Yondani, Erasto Nyoni, Haroub Nadir, Mwinyi Kazimoto,
Frank Domayo, Mrisho Ngasa, Khamis Mchana, Amri Kiemba, Salum Abubakar,
Simon Msuva, John Bocco, Vincent Barnabas, Mudathiri Yahya, Athuman Idd
na Haruni Chanongo.
Mechi ya marudiano itachezwa kati ya
Julai 26 na 28 mwaka huu kwenye Uwanja wa Nelson Mandela ulioko Namboole
nje kidogo ya Jiji la Kampala. Tarehe rasmi itapangwa na Shirikisho la
Vyama vya Mpira wa Miguu vya Uganda (FUFA) siku kumi kabla ya mechi.
TENGA AWASHUKURU WAJUMBE WA MKUTANO MKUU TFF
Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Leodegar Tenga amewashukuru wajumbe wa Mkutano Mkuu kwa michango yao, na utulivu waliouonesha katika kupitisha marekebisho ya Katiba ya TFF ya 2013.
Amesema marekebisho hayo yatawasilishwa kesho (Julai 15 mwaka huu) kwa Msajili wa Klabu na Vyama vya Michezo kwa ajili ya kupitishwa ili mchakato wa uchaguzi uweze kuanza mara moja.
“Tutamuomba Msajili atusaidie kusajili haraka Katiba yetu ya 2013 ili tuingie katika mchakato wa uchaguzi. Kama tulivyotangaza awali tumepanga kufanya uchaguzi Septemba 29 mwaka huu, na tusingependa tarehe hiyo ipite,” amesema Rais Tenga wakati akizungumza na Waandishi wa Habari mara baada ya kikao cha Kamati ya Utendaji.
Katika kikao chake, Kamati ya Utendaji imepitisha Kanuni za Maadili, Kanuni za Nidhamu, na marekebisho kwenye Kanuni za Uchaguzi yanayotokana na kuundwa kwa Kamati ya Maadili.
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
No comments:
Post a Comment