Kampuni ya simu za mkononi Vodacom Tanzania imetoa hundi yenye thamani ya shilingi milioni kumi, ikiwa ni mchango wa kuunga mkono jitihada za serikali katika kufanikisha zoezi la kuwasha na kuzindua mbio za mwenge wa uhuru, utakaozinduliwa rasmi mkoani Kagera Mei 2, mwaka huu.
Akizungumza wakati wa kukabidhi msaada huo meneja mawasiliano ya nje wa Vodacom, Salum Mwalimu amesema kuwa kutolewa kwa mchango huo kumetokana na ombi la mkuu wa mkoa wa Kagera kanali mstaafu Fabian Massawe alilolitoa kwa mkurugenzi mkuu wa Vodacom ili kufanikisha zoezi hilo.
Mwalimu amesema kuwa mchango uliotolewa na kampuni hiyo umelenga kutumika katika maeneo matatu ambayo ni kupamba uwanja wa Kaitaba ambako ndipo zitafanyika shughuli za kuwasha na kuzindua mwenge huo.
Amesema kuwa shughuli nyingine ni kutumika katika uhamasishaji wa wananchi kwa kutoa matangazo ili kuwawezesha kujitokeza kwa wingi kushiriki katika shughuli hiyo.
Amesema kuwa fedha hizo pia zinalenga kutumika katika matumizi ya simu za mkononi kwa kutoa ujumbe kwa wananchi kuhusiana na sherehe hizo.
Akipokea mchango huo leo (Mei Mosi mwaka huu) katika ofisi yake, mkuu wa mkoa wa Kagera kanali Massawe kwa niaba ya wananchi ameishukuru kampuni hiyo kwa mchango huo.
Amesema kuwa mwenge ni suala zuri lisilojali tofauti za kisiasa na kidini hivyo linapaswa kuungwa mkono na watu wote wapenda maendeleo.
Zaidi ya shilingi milioni 500 zinatarajiwa kutumika katika kukamilisha shughuli za kuwasha na kukimbiza mwenge huo ambao kauli mbiu yake mwaka huu ni katiba ni sheria kuu ya nchi, jitokeze kupiga kura ya maoni tupate katiba mpya.
No comments:
Post a Comment