BUKOBA SPORTS

Tuesday, August 19, 2014

KLABU YA SPORTING LISBON YATHIBITISHA MARCOS ROJO KWENDA MANCHESTER UNITED HUKU WAKIPEWA LUIS NANI KWA MKOPO!


KLABU ya Ureno Sporting Lisbon imethibitisha kuwa wao na Manchester United wamekubaliana Uhamisho wa Beki kutoka Argentina Marcos Rojo kwenda Man United na Nani kutua huko Lisbon kwa Mkopo wa Msimu mmoja.
Sporting Lisbon wao ndio walikuwa wa kwanza kuanika habari hizi kwa njia ya Mtandao wa Twitter wakithibitisha Rojo kwenda Old Trafford na Nani, Winga wa Man United aliehamia hapo kutoka Sporting Lisbon Mwaka 2007, kurudi kwao kwa Mkopo wa Mwaka mmoja.

Hivi punde, Klabu ya Man United imethibitisha Dili hii na kusema itakamilika baada ya upimwaji afya Rojo na makubaliano ya maslahi binafsi.
Awali Rojo alithibitisha kuhamia Man United hata kabla habari hizi kutolewa na Sporting Lisbon na pia kusema anatarajia Leo hii kusafiri kwenda Jijini Manchester.
Mapema Rojo alikaririwa kusema: “Ni kama ndoto kuwa Mchezaji wa Manchester United! Kuhama Sporting haikuwa rahisi!”

Hivi sasa pia zimeibuka ripoti kuwa Rojo aliisapoti Picha yake na Di Maria iliyowekwa kwenye Mtandao wa Instagram wakikumbatiana mbele ya Nembo ya Man United ikiwa ni ishara ya wazi kuwa wawili hao wako njiani kutua Old Trafford.

Rojo alihamia Sportung Lisbon Mwaka 2012 akitokea Spartak Moscow na Kampuni ya Doyen Sport ililipa Asilimia 75 na Sporting Lisbon kulipa Asilimia 25 ya Ada ya Uhamisho wake.
Rojo alicheza Mechi zote za Argentina huko Brazil kwenye Fainali za Kombe la Dunia ambapo Argentina ilifungwa kwenye Fainali Bao 1-0 na Germany na Meneja wa Man United, Louis van Gaal, anamwona Beki huyo ni kiraka kwenye Mfumo wake wa 3-5-2 kutokana na uwezo wake wa kucheza Sentahafu au Fulbeki wa Kushoto.
Beki huyo yumo kwenye Timu ya FIFA ya Fainali za Kombe la Dunia za Brazil 2014.
Kabla kuhamia Spartak Moscow na kisha Sporting Lisbon, Rojo aliichezea Estudiantes ya Argentina na kutwaa Copa Libertadores Mwaka 2009.

Nani Akiwa kwenye picha na  Sir Alex Ferguson na Owen Hargreaves miaka 7 iliyopita

No comments:

Post a Comment