BUKOBA SPORTS

Sunday, February 1, 2015

JEMBE JIPYA GABRIEL PAULISTA UWANJANI LEO ARSENAL vs ASTON VILLA


Kocha wa Arsenal, Arsene Wenger, amedokeza kuwa Beki wao mpya kutoka Brazil Gabriel Paulista ataanza Benchi kwenye Mechi yao ya Ligi Kuu England Uwanjani Emirates watakapocheza na Aston Villa leo Jumapili.
Paulista, mwenye Miaka 24, alikamilisha Uhamisho wake kutoka Villareal ya Spain Wiki hii kwenye Dili ambayo Straika wa Arsenal, Joel Campbell, alienda Villareal kwa Mkopo na kuwagharimu Arsenal Pauni Milioni 11.5.
Akimwelezea Paulista, Wenger amesema Paulista mwenye Urefu wa Futi 6 Inchi 2, ana ari na umbo zuri la kufanikiwa kucheza Soka la England na pia ana uwezo wa kucheza Fulbeki wa Kulia na Kushoto.

Wenger amesema: “Gabriel yuko tofauti na David Luiz ambae ni rahisi kumchukulia kama Kiungo Mkabaji badala ya Sentahafu. Gabriel ni Beki halisi. Yeye anatoka Sao Paolo. Ni Paulista wa kweli. Huko Brazil una Wachezaji wa Rio na unao Wachezaji wa Sao Paolo. Rio ni Bichi na Sao Paolo ni Wachezaji wachapa kazi!”

Hata hivyo, Paulista hazungumzi neno hata moja la Kiingereza na Kihispania chake ni cha kubabaisha na Wenger, ambae anazungumza Lugha nyingi lakini si Kireno anachoongea Paulista, amemtaka Mbrazil huyo kuongeza juhudi ya kujifunza Kiingereza.

Wenger ameeleza: “Haongei Kiingereza na hilo linaweza kukufungisha. Anacheza nafasi ambayo ni muhimu kujua Kiingereza ili ashirikiane vyema na wenzake. Tumeanza kumfundisha maneno muhimu kama vile ‘Ofsaidi’ na ‘Mtazame Mshika Kibendera.’”

No comments:

Post a Comment