Kikosi cha Timu ya Yanga
YANGA inaleta heshima kwa Watanzania. Yanga tamu mwe! Hayo yote unaweza kuyatumia kutamka ushindi wa mabao 2-0 iliyoupata Yanga dhidi ya BDF XI kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Yanga ilianza kuhesabu bao dakika ya kwanza, mfungaji akiwa Mrundi Amis Tambwe kwa kichwa kutokana na mpira wa kona uliopigwa na Haruna Niyonzima.
Dakika 20 za mwanzo BDF XI inayomilikiwa na Jeshi la Botswana, ilionekana kuzidiwa na wachezaji wa timu hiyo kujilinda zaidi badala ya kushambulia, hali iliyowapa mwanya Yanga kupanga mashambulizi.
Hata hivyo, washambuliaji wa Yanga, mara kadhaa walifika langoni, lakini walikosa umakini na kujikuta wakipiga juu ama kupiga michomo dhaifu iliyodakwa na kipa.
Dakika hizo 20 za mwanzo BDF XI ilifanya shambulizi moja la nguvu, wakati Master Mastara alipoingia eneo la hatari, lakini alipiga shuti lililopaa juu.
Kipindi cha pili kilianza kwa Yanga kushambulia kwa kasi, huku BDF XI wakionekana kupoteza muda zaidi kwa kuhitaji matokeo yabaki kama yalivyo.
Lakini dakika ya 56 Tambwe alifunga bao la pili kwa kichwa akiunganisha krosi ya Mrisho Ngassa, bao ambalo lilionekana kuwachanganya wachezaji wa BDF XI.
Dakika ya 64, 65 na 67 lango la BDF XI lilikuwa katika hekaheka, lakini Nadir Haroub, Andrey Coutinho na Haruna Niyonzima kwa nyakati tofauti walishindwa kutumbukiza mpira wavuni.
Yanga: Ally Mustapha, Mbuyu Twite, Oscar Joshua, Kelvin Yondani, Nadir Haroub, Salum Telela, Simon Msuva, Haruna Niyonzima, Amissi Tambwe/Jerry Tegete, Mrisho Ngassa na Andrey Coutinho/Kpah Sherman
No comments:
Post a Comment