BUKOBA SPORTS

Monday, June 29, 2015

KIPA PETR CECH AJIUNGA NA KLABU YA ARSENAL

Petr Cech akimwaga wino.
Petr Cech Leo amekamilisha Uhamisho wake wa kwenda Arsenal kama ilivyothibitishwa na Chelsea na yeye kuonekana akiwa na Jezi ya Arsenal huku akisaini Mkataba kufuatia Uhamisho wa Pauni Milioni 10.
Cech, mwenye Miaka 33, ameihama Chelsea baada ya kuitumikia Miaka 11 alipohamia kutoka Rennes ya France Mwaka 2004 na kuisaidia Chelsea kutwaa Ubingwa wa kwanza wa England baada ya Miaka 50 katika Msimu wa 2004/05.
Akiwa na Chelsea, Cech ameidakia Mechi zaidi ya 300 na kutwaa Ubingwa wa Ligi Kuu England mara 4, FA CUP 4, Kombe la Ligi
mara 3, UEFA CHAMPIONS LIGI na EUROPA LIGI mara moja moja.
Msimu uliopita Kipa wa Kimataifa wa Belgium, Thibaut Courtois, mwenye Miaka 23, alimpora Jezi Namba 1 Cech huko Chelsea na Cech kuruhusiwa kutimka na Mmiliki wa Chelsea, Roman Abramovic, na sasa amekuwa Mchezaji wa kwanza kusainiwa na Arsenal katika kipindi hiki.

Petr Cech anakuwa Mchezaji wa 6 kuhama moja kwa moja kutoka Klabu pinzani za Chelsea na kwenda Arsenal kufuatia Bill Dickson (Mwaka 1953), George Graham (1966), William Gallas (2006), Lassana Diarra (2007) na Yossi Benayoun (Mkopo, 2011).
Kutua kwa Cech huko Arsenal sasa kutamng'oa Kipa wa Colombia David Ospina ambae alihamia hapo toka Nice ya France Mwaka Jana huku Klabu ya Uturuki Fenerbahce ikitaka kumsaini.
Kipa mwingine wa Arsenal ni Wojciech Szczesny, anaetoka Poland, ambae amesema yeye atabaki Arsenal kupigania namba yake.
Mechi ya kwanza kwa Petr Cech inaweza kuwa dhidi ya Chelsea hapo Agosti 2 Uwanjani Wembley Jijini London kugombea Ngao ya Hisani wakati Arsenal itakapocheza na Chelsea katika mechi ya kufungua pazia Msimu mpya wa 2015/16.

No comments:

Post a Comment