Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akitazama ngoma baada ya kuwali kwenye uwanja wa ndege wa Bukoba kwa ziara ya kikazi mkoa wa Kagera Machi 13, 2016.(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemwagiza Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Bw. Hamad Masauni aimarishe udhibiti katika idara ya uhamiaji kwa kuwasimamia kwa karibu Afisa Uhamiaji wa Mkoa wa Kagera pamoja na maafisa uhamiaji wa wilaya za mipakani.
Ametoa agizo hilo leo mchana (Jumapili, Machi 13, 2016) wakati akitoa maelekezo baada ya kupokea taarifa ya mkoa wa Kagera ambako amewasili leo kwa ziara ya siku tatu kwa ajili ya kukagua masuala ya wakimbizi pamoja na mwenendo wa ranchi zilizo chini ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi na jinsi zinavyotumika.
“Idara ya Uhamiaji umakini wenu katika mkoa huu bado ni mdogo. Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani eneo hili ni lazima liimarishwe. RIO na DIO wa wilaya zote lazima mbadilike. Mmejisahau na mmesahau wajibu wenu wa kuilinda nchi. Ni lazima mbadilike mara moja,” alisema.
“Mmesahau kuwa watu wetu wanapaswa kulindwa na kuishi kwa usalama, badala yake kila mara tunasikia watu wakiuawa. Wizara ya Mambo ya Ndani kitengo cha Uhamiaji tutakiangalia mara mbili mbili ili kudhibiti hali hii,” alisema.
Alisema wilaya za Misenyi, Kyerwa na Ngara zimekithiri kwa udhaifu mkubwa wa kuleta raia kutoka nje na kuwaruhusu wafanye kazi za Watanzania na kuitaja wilaya ya Birahamulo kwamba yenyewe ina tatizo kama hilo lakini ni kwa kiwango kidogo.
“Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa nataka mhakikishe kuwa mkoa wa Kagera siyo eneo la kuingilia wavamizi. Kama ni watu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki tunao utaratibu wa jumuiya hii ya kutoa vibali kwa watu wake, nao ni lazima ufuatwe,” alisisitiza.
Waziri Mkuu alisema anazo taarifa kuwa mifugo ya kutoka nchi jirani inaingizwa hapa nchini na kunenepeshwa katika ranchi za taifa na kisha inarudishwa kwao kuuzwa. “Hivi ni kwa nini nyama ya ng’ombe wa Tanzania haina ubora wa kuuza kwenye masoko ya nje halafu sisi tunaruhusu watu wa nje waje wafaidike na rasilmali zetu?” alihoji.
“Ng’ombe anayeswagwa kutoka Kagera hadi Kilosa atakuwa na nyama nzuri huyo? Ng’ombe anayeswagwa na kuchapwa fimbo kutoka Itilima hadi Rufiji; je ngozi yake itakuwa nzuri hadi ipate thamani ya kuuzwa nje ya nchi?” alihoji na kuibua minong’ono miongozi mwa viongozi wa mkoa huo waliokuwa wakimsikiliza.
“Inasikitisha kuona mkoa huu una ranchi za kutosha lakini hazitumiki kwa manufaa ya wananchi wa mkoa huu. Mkuu wa Mkoa tumekupa dhamana ya kuongoza mkoa huu. Ukiona mmojawapo wa wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa ambao hawatimizi wajibu, waripoti kwa mamlaka za juu ili hatua za kinidhamu zichukukuliwe mara moja,” alisema.
Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kuhimiza makusanyo ya kodi kwenye ngazi ya Halmashauri ili kukuza pato la Taifa. “Ninawasihi Halmashauri mhakikishe mnakusanya mapato katika vyanzo mlivyovianisha na pia muwe waaminifu katika matumizi ya fedha hizo,” alisisitiza.
Mapema, akisoma taarifa ya mkoa huo mbele ya Waziri Mkuu, Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Bw. John Mongella alisema mkoa huo una eneo la hekta 176,000 ambazo ni za ranchi tu; maeneo ambayo alisema ni nyeti kiuchumi na kiusalama kwa sababu yamekaa mipakani.
Alitaja tatizo la wakimbizi kutoka nchi jirani kama changamoto nyingine kubwa ambayo inaikabili mkoa huo.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMAPILI, MACHI 13, 2016.
No comments:
Post a Comment