BUKOBA SPORTS

Friday, April 29, 2016

MASHABIKI WA ARSENAL BADO WAMEMKALIA KOONI MENEJA ARSENE WENGER, JUMAMOSI ARSENAL KUCHEZA NA NORWICH

Arsene Wenger amewasihi Mashabiki wa Arsenal kuwa kitu kimoja na kusema kuipinga Timu toka Majukwaani Uwanjani huathiri Timu yao Uwanjani.
Wadau wa Arsenal wamekuwa wakimpinga Wenger na kumtaka ang’oke kama Meneja baada ya kuona kwa mara nyingine tena wakianza vyema Msimu lakini baadae Timu ikisambaratika kwenye mbio za Ubingwa.
Wenger, ambae alitwaa Ubingwa wa England akiwa na Arsenal mara 3 na ya mwisho ikiwa 2004, amekiri kuelewa huzuni ya Mashabiki.
Lakini amesisitiza kuwa wapo Wachambuzi ambao hurubuni Mashabiki ili kusapoti upinzani ndani ya Klabu kwa maslahi na chuki zao binafsi.

Jumamosi, Arsenal wako kwao Emirates kucheza na Norwich City Mechi ambayo ni muhimu kwao kujihakikishia kuwemo 4 Bora za Ligi Kuu England ili kucheza UCL, UEFA CHAMPIONS LIGI Msimu ujao.
Kwenye Mechi hiyo, lipo kundi la Mashabiki wa Arsenal ambao wamepanga ‘kuandamana’ ili kuonyesha kupinga kwao uendeshwaji wa Klabu.
Wenger, akiongelea Mechi na Norwich na pia mipango hiyo ya Mashabiki Wapinzani, ameaasa: “Njia bora kwa Mashabiki ni kuwa nyuma ya Timu. Kuna Makundi yanataka kurubuni Mashabiki wetu, na naamini hii ni ajenda yao, ajenda binafsi, ya chuki binafsi.”
Aliongeza: “Ikiwa Klabu haiwezi kufurahia kitu chochote, basi ni mashaka. Kwenye Soka, unaporomoka haraka na unapanda polepole! Lazima tuwe kitu kimoja!”

No comments:

Post a Comment