Harakati za usajili jana zilishika kasi wakati klabu ya Yanga ilipopata ‘pigo la mwaka’ baada ya mtikisaji wake nyavu, Didier Kavumbagu (pichani) kutia wino kwenye fomu za mabingwa wapya wa soka nchini, Azam FC.
Nahodha huyo wa Burundi alionekana mwenye furaha na kuahidi makubwa, ingawa alikuwa na malalamiko kwa klabu ya Yanga.
“Mpira ni kazi yangu, sikuwa na uhakika wa wapi nitacheza kutokana na kumalizika kwa mkataba wangu,” alisema mshambuliaji huyo Mrundi ambaye alipachika mabao 10 msimu huu na kuiongoza Yanga kushika nafasi ya pili.
“Niliwapa Yanga nafasi, lakini hawakuonyesha kama wananihitaji. Sasa nimeamua kujiunga na Azam. Naomba ushirikiano.”
Kavumbagu alitoa siku tatu kwa uongozi wa Yanga kuamua hatima yake, lakini hakuna lililofanyika na wakati huo Azam FC, ambao watashiriki Ligi ya Mabingwa wa Afrika mwakani, walikuwa wakimnyemelea.
Kwa muda mrefu sasa, Kavumbagu na uongozi wa Yanga wamekuwa wakivutana kuhusu kuongeza mkataba wake baada ya mkataba wa sasa wa miaka miwili kumalizika. Lakini uongozi wa Yanga ulikaa kimya kuzungumzia suala hilo kutokana na kusubiri hatima ya sheria inayodhibiti idadi ya wachezaji wa kigeni.
Hata hivyo, mapendekezo ya kupunguza idadi ya wachezaji wa kigeni kutoka watano hadi kufikia watatu, haina budi kupitishwa na Kamati ya Utendaji ya TFF ikiwa ni utekelezaji wa maazimio ya Bagamoyo.
Kabla ya Kavumbangu kumwaga wino Azam, Yanga ilikuwa na wachezaji watano wageni. Wengine ni Mbuyu Twite, Emmanuel Okwi, Haruna Niyonzima na Hamis Kiiza ambao mikataba yao haijamalizika katika timu hiyo. Akizungumza na gazeti hili, meneja wa Azam FC, Jemedari Said alisema wameingia mkataba wa mwaka mmoja na Kavumbagu.
Said alisema hatua ya kumsajili Kavumbagu imetokana na mapendekezo ya kocha wao, Patrick Omong
“Ni mchezaji mzuri, lakini hakuwa anajua hatima yake. Ameichezea Yanga kwa miaka miwili na hakukuwa na mpango wowote wa kuendelea kuwa naye. Tulifanya naye mazungumzo na leo (jana) tumekamilisha suala lake,” alisema Said.
No comments:
Post a Comment