Katika mechi hiyo, Yassin alifunga mabao mawili na Okwi akifunga moja huku akitengeneza mengine mawili na Laudit Mavugo akifunga bao la nne kwa Simba.
Ni kama Okwi anawanyoosha mashabiki wanaomkebehi kwamba amezeeka na kumuita Mhenga, kwani mpaka sasa amefunga mabao nane huku timu yake ikiwa na mechi saba.
Matokeo hayo yanaifanya Simba inayohaha kusaka ubingwa kwa takribani mwaka wa tano sasa, kujikita kileleni mwa msimamo ikiwa na pointi 15 baada ya kucheza mechi saba.
Okwi alifunga bao la kuongoza kwa Simba katika dakika ya 27 baada ya kuunganisha mpira wa krosi ya Erasto Nyoni kabla ya kuujaza mpira wavuni akiwa amefikisha bao la nne msimu huu.
Simba iliyoonekana kuwa bora zaidi kwani ilifika langoni mwa Njombe Mji mara kwa mara huku wachezaji wake akiwemo Shija Kichuya wakikosa mabao kadhaa na kwenda mapumziko wakiwa mbele kwa bao hilo.
Njombe walianza kipindi cha pili wakiwa dhaifu zaidi ya kipindi cha kwanza na hapo safu ya ushambuliaji ya Simba haikufanya kosa na ndipo Mzamiru Yassin alipoandika bao la pili katika dakika ya 51 na dakika mbili baadae aliongeza la tatu. Mabao yote hayo akiunganisha pasi za ‘Mhenga’ Okwi.
Dakika ya 59, Laudit Mavugo alifunga bao la nne akiunganisha pasi ya Kichuya.
Baada ya mechi ya leo, Simba kesho itafanya safari ya Zanzibar kwa maandalizi ya mechi dhidi ya Yanga Jumamosi.
Naye Alexander Sanga kutoka Mwanza anaripoti kuwa Mbao imetoka suluhu na Azam kwenye uwanja wa CCM Kirumba.
Mechi nyingine zilizochezwa jana, Lipuli ikiwa nyumbani imeichapa Majimaji bao 1-0 Mbeya City imeifunga Ruvu Shooting mabao 2-0 kwenye uwanja wa Sokoine Mbeya, Ndanda ikitoka suluhu na Singida United na Mtibwa Sugar ikishinda bao 1-0 dhidi ya Prisons.
Mtibwa imeendelea kushika nafasi ya pili kwenye msimamo ikiwa pointi sawa na Simba, ikizidiwa mabao.
No comments:
Post a Comment